Wimbi la majonzi lilitanda katika eneo la Kinango, Kaunti ya Kwale wakati Mhubiri Spencer Mdave alipokuwa akizika wanawe wanne Salem, Sharon, Sarah, na Shekinah walioaga dunia kwenye ajali katika barabara kuu ya Mombasa–Nairobi eneo la Kanga wiki mbili zilizopita. Wanne hao walizikwa katika kaburi moja Jumatano. Ndugu hao wanne waliaga dunia kwenye ajali iliyosababisha maafa ya watu 25 baada ya basi walimokuwa wakisafiria kutoka mazishi ya jamaa yao Lugari, Kaunti ya Kakamega kugongana ana kwa ana na lori katika eneo la Kanga.
Basi hilo lilikuwa limebeba abiria 50, wakiwemo jamaa wa karibu, waumini wa makanisa mbalimbali, na wachungaji 12 waliokuwa wakirejea Mombasa. Mhubiri Spencer Mdave, ambaye alinusurika kwenye ajali hiyo, alisema alijaribu kuwaokoa wanawa lakini hakufua dafu. “Salem, wewe ndiye mtoto wetu wa kwanza ambaye ulitufanya tukaitwa wazazi kwa mara ya kwanza. Baba yako alikuwepo eneo la ajali na alishuhudia yasiyofajirika.
Mhubiri huyo alisema aliwaombea wanawe Sharon na Sarah, pindi baada ya ajali. “Baba yenu aliomba nanyi, akishikilia imani na kutumaini muujiza. Alijisalimisha kwa Mungu kwa maomba si kama mchungaji, bali kama baba yenu aliyetamani kwa dhati binti zake wangeliishi,” risala ya wazazi hao ikaeleza. Kuhusu kitinda mimba yao Shekinah, wazazi hao walilia ndoto zake zilizokatizwa kwa ghafla.
Akihutubia mkusanyiko huo, Bw Mdave alieleza shukrani zake kwa majirani, waumini wa kanisa, na viongozi waliounga mkono familia hiyo wakati wa tukio hilo hadi mazishi. “Wengi wa jamaa zangu walijeruhiwa katika ajali hiyo, na wengine waliangamia. Lakini tunamshukuru Mungu kwa sisi tulionusurika; tuko hapa kumtukuza Mungu kwa kila jambo.
Viongozi wa kisiasa wa eneo hilo, wakiongozwa na Naibu Gavana wa Kwale Chirema Kombo, waliwapongeza mawaziri Bw Hassan Joho na mwenzake Salim Mvurya kwa kuwasaidia kifedha familia hiyo. Katika Kanisa la ACK Mombasa Memorial Cathedral, Askofu Mkuu Alphonse Baya aliongoza ibada ya misa ya kuwakumbuka waathiriwa wengine wanne kutoka familia moja waliangamia katika ajali hiyo hiyo.
Wanne hao walizikwa jana katika kijiji cha Mikomani, Rabai, Kaunti ya Kilifi. Marehemu Younitta alihudumu kama mwenyekiti wa kwanza wa kamati ya mipango mkakati ya kanisa hilo mnamo 2018. “Leo ni siku ya huzuni sana. Nimepoteza mtaalamu aliyejitolea kufanya kazi kwa ajili ya kanisa na jamii,” alisema Askofu Baya.
Kiongozi huyo wa dini alionya kuwa barabara kuu za nchini zimegeuka kuwa maeneo ya maombolezo kwa familia nyingi. Katika mazishi na misa zote za wafu, waliohutubu walirejelea kusisitiza wito kwa serikali ichukue hatua kuepusha ajali mbaya zinazotokea mara kwa mara katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi.
Key points
- Mhubiri Spencer Mdave amezika wanawe wanne waliofariki katika ajali ya barabara Kanga.
Reporting sources
- Majonzi tele mhubiri akizika wanawe 4 waliofariki ajalini Kanga · taifaleo.nation.co.ke