Ajali ya kutisha ilitokea Ijumaa, Novemba 13, 2026, katika eneo la Bandari ya New Orleans, Louisiana, nchini Marekani, wakati meli kubwa ya kubeba mafuta aina ya tanker kuigonga meli ya kitalii ya American Heritage. Meli hiyo iliyomilikiwa na kampuni ya American Cruise Lines ilipinduka na kuzama kwa sehemu, na abiria wakijikuta ndani ya maji na wengine wakihangaika kushikilia sehemu za meli ili kujiokoa.
Meya wa New Orleans, Helena Moreno, alisema takribani abiria na wafanyakazi 180 hadi 190 walikuwa ndani ya meli hiyo wakati ajali inatokea. Alithibitisha kuwa watu wote waliokuwa ndani ya meli hiyo wamepatikana, huku watu 32 wakipelekwa hospitalini kwa matibabu kutokana na majeraha waliyopata. Hata hivyo, hakuna aliyeripotiwa kuwa katika hali mbaya inayotishia maisha.
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha tanker hiyo ikiikaribia meli ya kitalii kabla ya kuigonga kwa nguvu, huku abiria wakionekana kukimbia kuokoa maisha yao wakati chombo hicho kikianza kupoteza mwelekeo na kuzama. Kapteni Melanie Burnham wa Walinzi wa Pwani ya Marekani alisema uchunguzi wa awali unaashiria kuwa tanker hiyo huenda ilipata hitilafu katika mfumo wa usukani na kushindwa kudhibiti mwelekeo wake.
Taarifa zinaeleza kuwa polisi wa bandari, wazima moto, polisi wa jiji na maafisa wa Walinzi wa Pwani wa Marekani walishiriki katika zoezi la uokoaji. Pia, watu waliokuwa kwenye vyombo vingine vya majini walijitokeza kusaidia kuwatoa abiria waliokuwa wameangukia majini. Juhudi za waokoaji zifanikiwa kuwanusuru watu wote bila kuripotiwa vifo.
Kampuni ya American Cruise Lines imesema inashirikiana na mamlaka husika katika kushughulikia tukio hilo na kuthibitisha kuwa abiria pamoja na wafanyakazi wote wameokolewa. Bodi ya Taifa ya Usalama wa Usafiri (NTSB) ikianza uchunguzi kubaini kilichosababisha tukio hilo. Chanzo rasmi cha ajali hiyo bado hakijathibitishwa.
Mmoja wa wafanyakazi wa mgahawa wa meli hiyo alieleza kuwa tukio hilo lilisababisha hofu kubwa miongoni mwa abiria, hasa baada ya kuona maji yakiingia ndani ya eneo la mgahawa kupitia sehemu iliyoharibika kutokana na mgongano. Tukio hilo limeibua maswali kuhusu usalama wa vyombo vya majini na sababu zilizofanya tanker kubwa kushindwa kudhibiti mwelekeo wake na kugonga meli nyingine iliyokuwa imetia nanga bandarini.
Mamlaka za eneo hilo zimeendelea kutoa taarifa za hivi punde kuhusu tukio hilo, huku wakihakikisha kuwa uchunguzi utafanyika kwa umakini ili kubaini chanzo cha ajali hiyo. Kufikia sasa, hakuna taarifa rasmi kuhusu chanzo cha ajali hiyo, lakini uchunguzi unaendelea.
Key points
- Abiria 32 wakimbizwa hospitalini kufuatia ajali ya meli katika Mto Mississippi.
- Meli ya kitalii ya American Heritage ilipinduka na kuzama kwa sehemu baada ya kugongwa na tanker.
- Uchunguzi wa awali unaashiria hitilafu katika mfumo wa usukani wa tanker kama chanzo kinachowezekana cha ajali.