Kasi ya mabadiliko ya teknolojia nchini Tanzania inaendelea kuongeza chachu katika sekta mbalimbali za uzalishaji na biashara. Kampuni zinajikita zaidi kwenye ubunifu, kuboresha huduma kwa wateja, na kudumisha ubora wa bidhaa ili kuendelea kuwa na ushindani sokoni. Mabadiliko haya ya teknolojia yamekuwa yakichochea uzalishaji wa bidhaa zinazoleta suluhisho na kukidhi matarajio yanayobadilika ya watumiaji.
Wadau mbalimbali wanasema kuwa kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia, hususan akili mnemba (AI), ni muhimu kwa kampuni zinazotaka kuendelea kuwa na nafasi katika soko. Mkurugenzi wa Masoko wa MeTL Group, Fatema Dewji, alisema biashara zitakazoshindwa kuendana na maendeleo ya kiteknolojia zinaweza kuachwa nyuma. Ubunifu unaendelea kuwa na nafasi kubwa katika uuzaji, usambazaji, na uundaji wa bidhaa.
Fatema Dewji alisema hivyo wakati wa hafla ya mashirikiano baina ya MeTL Group na Haier Tanzania. Ushirikiano huo unakuja wakati ushindani katika soko la vifaa vya matumizi ya nyumbani unapozidi kutegemea uwezo wa biashara kuunganisha ubunifu wa kiteknolojia na ubora wa bidhaa ili kutimiza mahitaji ya walaji.
Fatema Dewji aligusia juu ya mitazamo ya watu kuhusu AI, ambapo wengi wanaitazama kama ni tishio kwenye soko la ajira. Hata hivyo, alisema licha ya nguvu yake, bado ubunifu na mawazo ya binadamu vitaendelea kuwa muhimu hata wakati biashara zikiongeza matumizi ya teknolojia mpya. Teknolojia hii haiwezi kuchukua nafasi ya mawazo au watu wenye ubunifu na fikra.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia, hususani akili bandia, yameendelea kuongeza chachu kwenye utendaji kazi. Ujuzi na ubunifu kwenye sekta hiyo unazidi kuwa muhimu katika kupata ajira za sasa na zijazo. Hivi karibuni, Serikali ilisema kuwa itaendelea kuhamasisha matumizi ya akili bandia ikiwa ni jitihada za kuboresha ufanisi na kuongeza tija mahali pa kazi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Elimu, Dkt Hussein Mohammed Omari, alisema watu wanaopata ujuzi wa kutumia AI kwa ufanisi wana uwezekano mkubwa wa kupata fursa zaidi za ajira katika soko la ajira linaloendelea kubadilika. Alitoa kauli hiyo mwezi uliopita wakati wa kufunga mkutano wa 42 wa Chama cha Tathmini ya Elimu Afrika (AEAA).
Meneja wa Haier-Tanzania, Liu Chi, alisema soko la vifaa vya matumizi ya nyumbani hapa nchini linaendelea kubadilika. Watumiaji wengi sasa wanaangalia zaidi ubora wa bidhaa, hivyo kama kampuni zinawajibu wa kuhakikisha zinazalisha bidhaa zenye tija ili kufikia mahitaji ya walaji.
Key points
- Matumizi ya AI yameendelea kuchochea uzalishaji na biashara nchini Tanzania.
- Kampuni zinajikita kwenye ubunifu na kuboresha huduma kwa wateja ili kuendelea kuwa na ushindani sokoni.
- Serikali inahamasisha matumizi ya akili bandia ili kuboresha ufanisi na kuongeza tija mahali pa kazi.